Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI), Asseny Muro
(kushoto) akiwahutubia wahitimu wa mahafali ya pili ya chuo hicho leo
katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha GTI, Zuki Mihyo (wa pili kushoto) akitoa hotuba yake
kwa wanamahafali wa mafunzo ya jinsia katika chuo cha GTI leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI), Asseny Muro
pamoja na Mkuu wa Chuo cha GTI, Zuki Mihyo (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi
wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi (kulia) wakiongoza maandamano ya
wanamahafali ya pili ya Chuo cha GTI kuelekea ukumbuni kabla ya kuanza
kwa hafla hiyo.
Mkuu wa taaluma na mipango wa GTI, Bi Doroth akitamka kuanza kwa
sherehe za Mahafali ya Pili ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia Tanzania (GTI)
kwenye hafla ya mahafali hayo leo.
Sehemu ya wanamahafali wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) wakiwa
kwenye sherehe za mahafali yao yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano
wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) leo Mabibo jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia, Asseny Muro
(kushoto) akimtunuku cheti cha jinsia mmoja wa wahitimu wa mahafali ya
pili ya chuo hicho leo katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es Salaam
Mmoja wa wanamahafali wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) (kulia) akionesha cheti chake mara baada ya kutunukiwa.
Mmoja wa wanamahafali wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) (kulia)
akikabidhiwa cheti chake mara baada ya kutunukiwa na Mwenyekiti wa Bodi
ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia, Asseny Muro (kushoto)
Mmoja wa wanamahafali wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) (kulia) akionesha cheti chake mara baada ya kutunukiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi (kulia) akinong'ona
jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia, Asseny Muro
kwenye sherehe za mahafali ya pili ya Chuo cha GTI leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia, Asseny Muro, Mkuu wa
Chuo cha GTI, Zuki Mihyo, Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Mtandao, Lilian
Liundi na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wanamahafali baada
ya kutunukiwa vyeti vyao.
Wanamahafali wakiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza kwa sherehe za mahafali yao leo.
Na Thehabari.com, Dar es Salaam
MAHAFALI ya pili ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI)
yamefanyika leo jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo
hicho eneo la Mabibo. Katika sherehe hizo jumla ya wanafunzi 9
wamehitimu mafunzo ya njinsia ngazi ya cheti.
Akizungumza kabla ya kuwatunuku vyeti, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha
Mafunzo ya Jinsia, Asseny Muro alikipongeza chuo hicho kwa kuendelea
kutoa mafunzo ya jinsia nchini kwa ngazi mbalimbali jambo ambalo
linawezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kuchambua na kutathmini sera na
program anuai kwa mtazamo wa kijinsia katika sekta mbalimbali za
maendeleo.
Aliutaka uongozi wa GTI kwa kushirikiana na bodi kutatua changamoto
mbalimbali zinazokikabili chuo hicho, ikiwemo changamoto za uhaba wa
raslimali watu na fedha ili kuhakikisha malengo ya chuo hicho ya
kudahili wanafunzi wengi zaidi yanafikiwa na kuanza kwa wakati.
"..Rai yangu niwaombe wewe mkuu wa chuo kwa kushirikiana na bodi ya GTI
mfanye kila liwezekanalo ili kuwezesha mafunzo hayo kuanza mapema na
hatimaye wanafunzi hawa na wengine watakaopenda kuendelea na masomo yao
hapa chuoni wafanye hivyo ili kutimiza ndoto zao na matarajio yao,"
alisema Bi. Muro.
Aidha aliwapongeza wahitimu kwa kufanikiwa kumaliza mafunzo yao na
kuwataka wakaitumie elimu hiyo kiufasaha kwa jamii, ikiwa ni pamoja na
kuwa wataalamu na mabalozi wazuri wa masuala ya jinsia hapa nchini.
"...Nitumie fursa hii kuwaomba mkawe wataalamu na mabalozi wazuri wa
masuala ya jinsia hapa nchini na kwa kufanya hivyo nchi itajivunia
utaalamu wenu ambao kama utatumika vizuri utaiwezesha jamii kuwa na
mipango na utekelezaji wa shughuli za maendeleo...," alisisitiza.
Naye Mkuu wa Chuo cha GTI, Zuki Mihyo akizungumza na wahitimu na wageni
waalikwa kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi alisema chuo hicho
kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikikwamisha
utekelezaji wa mipango yake kikamilifu, hivyo kuiomba Bodi ya chuo
kusaidia kutatua changamoto hizo ili chuo kiendelee kufanya vizuri zaidi
katika mipango yake.
Mahafali hayo ya Chuo cha GTI ambacho kinaendeshwa na Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP) pia yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,
Mary Rusimbi, Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi,
wafanyakazi wa GTI na TGNP Mtandao pamoja na wageni waalikwa