Baadhi ya waandishi wa habari na wadau kutoka asasi mbalimbali
nchini wakifanya usajili kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa
kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini
Arusha.(Picha na Zainul Mzige).
Na Waandishi Wetu, Arusha
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF),
Absalom Kibanda ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuyapa uzito
matukio yanayowatokea waandishi wa habari na kuyapigia kelele kwa nguvu
zote ili kuyakomesha.
Kibanda aliyasema hayo jana mjini Arusha
katika kongamano lililoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya
uhuru wa vyombo vya habari duniani na kuongeza kwamba wakati umefika kwa
waandishi wa habari kuondoa tofauti zao na kuungana pamoja kuongeza
nguvu waliyonayo kukabiliana na ukatili unaoendelea dhidi ya waandishi
wa habari katika miaka ya hivi karibuni.
“Baadhi ya wahariri huwa hawayaandiki
madhila yanayowasibu waandishi wa habari na kuyapa uzito unaostahili
aidha kwa huyapuuzia au kudharau kwa kuwa hayawahusu moja kwa moja,”
alisema Kibanda.
Aliongeza kwa kusema kuwa vyombo vya habari
mara nyingi vimekuwa vikinyooshewa vidole na kulaumiwa kwa kutokufanya
kazi kwa uadilifu jambo ambalo linatafsiriwa kuwa ni la uonevu,
vinatumiwa vibaya na hakuna anayesimama kuvitetea kutokana na mchango
wake mkubwa katika jamii.
Afisa Mipango Kitengo cha Mawasiliano, Habari na Tehama UNESCO,
Bw. Al Amin Yusuph, akiwasilisha mada kuhusu mchango wa uhuru wa vyombo
vya habari katika utawala bora, kukuza uwezo na kupunguza umaskini
kongamano la waandishi wa habari lilioandaliwa kama sehemu ya
maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika
jijini Arusha.
“Kwa sasa tasnia hii iko kwenye wakati mgumu
sana kwani hata marais wa nchi mbalimbali mfano Uganda, Kenya hata
Marekani wanakinzana na vyombo vya habari kwa madai kuwa kauli zao
zinapotoshwa, laikini ukweli ni kwamba ni vyema kauli hizo za viongozi
zikachunguzwa kwa undani zaidi ili kuelewa iwapo zina uwajibikaji ndani
yake,” alisema Kibanda.
Kibanda aliongeza kuwa wakati umefika sasa
kwa waandishi kutambua kuwa kuna ajenda za siri zilizojificha dhidi ya
uteswaji wa waandhishi wa habari hivyo yasidharauliwe, yafanyiwe kazi
kwa kina ili kuelewa kiini cha tatizo kwa kupata ufumbuzi.
Kwa upande wake mwandishi mkongwe na
aliyetunukiwa tuzo ya maisha mwaka 2012 na Baraza la Habari Hamza
Kasongo alisema vyombo vya habari vina nguvu kubwa katika kushawishi
hivyo vitumie nguvu hiyo kama muhimili wa nne wa nchi katika kuzikabili
changamoto zilizopo.
“Kuwe na mtandao unaoeleweka wa mawasaliano
kati ya waandishi wa habari nchini ili kuhakikisha kuwa matatizo
yaliyopo yanatatuliwa bila woga na kwa ujasiri kwa lengo la kufanya
kazi kwa ufanisi mkubwa,” alisema Kasongo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria , Bw.
James Jesse, akitoa mada kuhusu umuhimu wa sheria katika kulinda haki
ya uhuru wa kujieleza kwa kila mtu wakati wa kongamano la waandishi wa
habari lilioandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa
vyombo vya habari duniani yanayofikia kilele leo jijini Arusha.
Mwanahabari mwingine mkongwe Dokta Samwilu
Mwaffisi aliyetoa mada ya Maadili ya Uandishi wa Habari alisema kuwa
kuna haja ya waandishi kuzingatia uhuru wa habari walionao kwa
kuzingatia maadili yanayowaongoza ili kuboresha heshima waliyonayo
katika jamii kwa kuandika ukweli na uhakika, bila upendeleo, kutoa fursa
ya kujitetea na kukubali kuomba radhi pale unapokosea.
“Kuandika habari zenye kuzingatia maadili
kunapunguza manung’uniko, mashauri na kuongeza heshima ya chombo cha
habari na mwanahabari mwenyewe,”
Akizungumzia suala la ufanisi, Rais wa
Vilabu vya Waandishi wa Habari, Kenneth Simbaya, aliwaasa waandishi wa
habari kusimamia ukweli katika kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa
mazoea jambo ambalo litakawaweka huru zaidi katika utekelezaji wa
shughuli zao za uandishi wa habari.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na umoja wa
asasi mbalimbali chini ya uenyekiti wa MISA TANZANIA unafikia kilele
chake tarehe 3 Mei kwa kuzindua majarida mbalimbali, matamko kutoka
asasi mbalimbali na kuhitimishwa kwa tafrija ya chakula cha jioni chini
ya mgeni rasmi Jaji Mstaafu Mheshimiwa Mark Bomani.
Mwanahabari Mkongwe kutoka Chuo Kikuu Huria, Dokta Samwilu
Mwaffisi (kulia) akiwasilisha mada ya Maadili ya Uandishi wa Habari
kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo
vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha. Kushoto ni Mhadhiri
kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Bw. Simon Berege.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, akitoa
maoni yake wakati wa kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha
Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Pichani juu na chini ni baadhi ya waandishi wa habari wakongwe,
mabalozi na wanahabari washiriki katika kongamano la siku moja
lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014
lililofanyika jijini Arusha.
Mwandishi wa Habari Chokonozi, Bw. Fredrick Katulanda, akielezea
madhila mbalimbali yaliyomsibu katika utekelezaji wake wa kuandika
habari za uchambuzi.
Mwanahabari Mkongwe Bi. Leila Sheikh akichangia mada ya Mchango
wa Uhuru Wa Vyombo Vya Habari Katika Utawala Bora, Kukuza Uwezo Na
Kupunguza Umaskini wakati wa kongamano la siku moja lilioandiliwa
kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini
Arusha.
Mmiliki wa Gazeti tando la Mjengwa na Kituo cha Redio Kwanza
Jamii, Bw. Maggid Mjengwa akielezea jinsi Intaneti inavyoweza
kuunganisha mtandao wa Redio.
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania
(COMNETA) na Mkurugenzi wa kituo cha mawasiliano Sengerema, Bw.
Felician Ncheye akichangia mada.
Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Mama Rose Haji Mwalimu, (kushoto) akiwa na baadhi ya washiriki wa Kongamamo hilo.
Rais wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Bw. Kenneth Simbaya, akishiriki kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Picha juu na chini Baadhi ya washiriki wakichangia maoni yao
kwenye kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo
vya Habari Duniani 2014 lililofanyika jijini Arusha.
Kongamano la siku moja lilioandiliwa kuadhimisha Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani 2014 likiendelea.
Mwanakamati wa maandilizi ya maadhimisho ya Kongamano la Uhuru
wa Vyombo vya Habari Duniani 2014, Usia Nkhoma Ledama wa Kitengo cha
Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda nje ya ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa AICC jijini Arusha