WANANCHI katika kijiji na kata ya Guta, wilaya ya Bunda mkoani Mara,
wamelalamikia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu katika kata
hiyo, kwa kufanya ngono na wanafunzi na kuishi nao kinyumba kama wake
zao.
Hatua hiyo ya kulaani inatokana na hivi karibuni kumkamata mwalimu wa
shule ye Msingi Guta, akiishi na mwanafunzi wa shule hiyo kinyumba kama
mkewe.
Wananchi wa kata hiyo wakiongozwa na diwani wao, Kigo Nyamhanga, jana
waliwaambia waandishi wa habari kwa njia za simu za mkononi kuwa hivi
karibuni katika kijiji cha Guta, walifanikiwa kumkamata mwalimu huyo
(jina linahifadhiwa) akiishi na mwanafunzi wa shule hiyo nyumbani kwake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti huku wakioneshwa kusikitishwa kwa
vitendo hivyo, walisema kuwa baadhi ya walimu wa shule za msingi na
sekondari, ambao hawazingatii maadili ya kazi yao, wamekuwa na tabia
hiyo chafu na mbaya ya kufanya vitendo vya ngono na wanafunzi wao.
Walisema hivi karibuni saa za usiku walimkamata mwalimu huyo
anayefundisha katika shule ya msingi Guta, akiwa na mwanafunzi mmoja
wakiishi naye nyumbani kwake kama mke wake.
Walisema kuwa walifanikiwa kumtia mbaroni mwalimu huyo baada ya kupata
taarifa kutoka kwa raia wema, kwamba mwalimu huyo anaishi na mwanafunzi
huyo nyumbani kwake na wanafanya naye vitendo vya ngono. Walisema kuwa
baada ya kumkamata polisi walifika na kumpeleka kituo kikuu cha polisi
cha wilaya hiyo.
“Baada ya wananchi hao walioongoza na mwenyekiti wa kijiji chao
walifanikiwa kumkamata live mwalimu huyo akiwa na mwanafunzi ndani ya
nyumba yake” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulsha kwa jina moja la
Juma, mwenyekiti wa CCM, tawi la Guta.
Diwani wa kata hiyo, Kigo Nyamhanga, alithibitisha tukio hilo na kusema
kuwa mwalimu huyo alikamatwa na wananchi walioongoza na mwenyekiti wa
kijiji hicho.
Kufuatia tukio hilo, diwani huyo alikemea tabia hiyo na kuwataka walimu
katika kata hiyo, kuachana na tabia hiyo chafu, kwani wao wanapewa
watoto kuwalea na kuwafundisha na siyo kuwafanyia ukatili huo wa
kijinsia.
Aliongeza kamwe tabia hiyo katika kata yake, haiwezi kuvumiliwa ndani ya jamii na hata serikali kwa ujumla
No comments:
Post a Comment