Majeneza yenye miili ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani
waliofariki dunia baada ya kugongwa na basi wakati wakipima ajali
katika kijiji cha Utaho wilani Ikungi mkoa wa Singida kabala ya kuagwa
na kusafirishwa kwenda makwao. Picha na Gasper Andrew
Singida. Wakati
miili 15 ya marehemu waliofariki dunia kwa kugongwa na basi katika
Kijiji cha Utaho mkoani Singida ikizikwa juzi, imeelezwa kuwa eneo hilo
limekithiri kwa ajali hadi kuwatisha wanakijiji.
Wakazi wa kijiji hicho walisema jana kuwa ndani ya miaka minne, zaidi ya
watu 50 wamepoteza maisha katika eneo hilo kutokana na ajali kiasi cha
kuingiza hisia za imani za kishirikina.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Selemani Kinanda alisema: “Kwa miaka
minne iliyopita, ukiacha marehemu 15 wa juzi, watu karibu 50 wamepoteza
maisha. Wengi ni vijana wa kiume.”
Alisema naye aliwahi kupata mikasa katika eneo hilo na kujikuta
amejibamiza kwenye gari na kuhama barabarani hadi kichakani na baiskeli
yake, baada ya kuona ‘mauzauza’ kwenye eneo hilo.
“Kwanza yule aliyegongwa kwanza na kusababisha yote haya hatujui
alitokea wapi, pia kulikuwa na sababu gani kwa dereva huyu wa basi
kuwafuata watu hao wote pembeni na kuacha barabara kubwa kulia kwake?
Hatukusikia gari ni bovu wala tairi limepasuka, lazima kuna mkono wa
mtu,” alisema Fatuma Shabani, aliyefiwa na kaka yake.
Hata hivyo, taarifa kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani zinasema kuwa
hakuna takwimu zozote zinazoonyesha idadi ya ajali au vifo katika eneo
hilo, zaidi ya ile ya juzi yenye takwimu sahihi.
Majonzi kijijini
Kijiji kizima cha Utaho tangu juzi kilikuwa katika majonzi na simanzi,
hata baada ya miili ya marehemu wanane wa ukoo mmoja na wengine saba
wahamiaji kutoka vitongoji vya Maguha na Kinyaghaa kuzikwa katika
makaburi ya kimila kijijini hapo.
Kutokana na familia nyingi kuwa na msiba, watu walionekana wakitoka nyumba moja kwenda nyingine kutoa pole.
“Msiba ulikuwa mgumu, tulikuwa tukichimba kaburi hapa tunazika,
tunakwenda kwa mwingine. Kilio hiki ni cha ajabu na miujiza sana kwetu,”
alisema Ramadhani Nyange (74) na kuongeza: “Tunashindwa tuanzie wapi au
kwa nani, maana sisi wote ni ndugu, tumeoleana na kuzaliana kutoka kwa
babu yetu Bulali Masuja ambaye ni mwanzilishi wa kijiji tangu mwaka
1972.”
Alisema kuna haja ya kufanya mkutano wa ukoo ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Watu hao ni miongoni mwa 19 waliokufa katika ajali hiyo wakiwamo
mwenyekiti wa kijiji, ofisa mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa
kitongoji pamoja na askari polisi wanne. Watu wengine wanane
walijeruhiwa.
Aidha, wananchi hao walionyesha wasiwasi juu ya shughuli za maendeleo
baada ya kufiwa na viongozi wote na juu ya Sh10 milioni za kijiji
zilizoko benki.
Mazishi ya polisi
Mazishi ya askari F 6837 PC Jumanne Mwakihaba yalifanyika jana saa 7:00
mchana katika makaburi ya Kisarawe Mjini, yakiongozwa na Mkuu wa Polisi
Wilaya ya Kisarawe (OCD), Issa Lutavi.
Mwili wa marehemu ulifikishwa nyumbani kwao Kisarawe alfajiri jana na
ulizikwa kwa taratibu za kijeshi. Mwakihaba alijiunga na jeshi hilo
Agosti 30, 2004 na kupangiwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani
Singida ambako mauti yamemkuta.
Habari zilizopatikana mkoani Kilimanjaro, zilisema kuwa mwili wa G. 7993 Novatus Tarimo utazikwa kesho huko Tarakea, Rombo.
Kikwete atuma salamu
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa
Singida, Dk Perseko Kone kutokana na ajali hiyo iliyosababisha vifo
hivyo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema jana kuwa
Rais amesikitishwa na ajali hiyo iliyopoteza nguvu kazi muhimu kwa
ujenzi wa Taifa.
“Vifo hivi hakika vimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa familia, ndugu,
jamaa na marafiki wa marehemu,” taarifa hiyo ilimkariri Rais Kikwete.
Pamoja na kuwahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza
msiba huo, Rais Kikwete aliwaombea kwa Mungu watu wote waliojeruhiwa
wapate kurejea haraka katika hali zao za kawaida
No comments:
Post a Comment