Dar/ Mikoani.
Wakati leo ni maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar uliozaa taifa la Tanzania, wasomi, viongozi wa dini, watendaji
wa Serikali na wananchi wa kawaida wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu
uhai wa Muungano huo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi walitaka
Muungano huo uvunjike kwa madai ya kutokuwa na manufaa yoyote, au uwe wa
Serikali moja, huku wengine wakitaka uenziwe kwa sababu ndiyo chachu ya
amani, umoja na mshikamano uliopo sasa.
Moshi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Padri Francis Shawa alisema:
“Muungano uendelee ila kuwe na serikali moja kama ilivyokuwa awali na
Rais akitoka Zanzibar makamu atoke Bara na kusiwe na marais wawili.”
Alisema wadhifa wa Rais wa Zanzibar na makamu wake viondolewe na pande
zote zikubali baadhi ya vitu kutoa sadaka kwa kuvipoteza.
“Nakerwa zaidi na Zanzibar kuwa na Katiba yao , wakati Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Zanzibar ni sehemu ya nchi yake
pia. Wakati wa Sherehe za Muungano, Rais wa Zanzibar ndiye anaonekana
mwenye nguvu, kitu ambacho siyo sahihi. Rais wa Tanzania ndiye apewe
hadhi kubwa,” alisema.
Diwani wa Kata ya Kilema Kusini, Kawawa Lubega alipendekeza Serikali
mbili na alitoa sababu kuwa hata Serikali mbili za sasa bado wananchi
hawajazifahamu vizuri. Lubega alisema kwamba shirikisho la serikali tatu
litasababisha Rais atakayekuwapo madarakani akose nguvu kiuchumi na
kiutawala.
Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari za Wilaya ya Moshi, George Jidamva
alipendekeza kuwapo kwa serikali mbili, lakini akashauri Katiba zote
mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, ziwekwe
mezani ili dosari zilizopo zirekebishwe akitaja kipengele cha madaraka
ya Rais.
Mwanasheria wa Serikali, Wilaya ya Moshi, Glorian Issagya alipendekeza
pia serikali mbili ziendelee, lakini akasema wabunge waliojitoa bungeni,
warudi ili changamoto zinazojitokeza ziweze kufanyiwa kazi zisije
zikaleta athari hapo mbeleni.
Songea
Naye mwanasiasa, Asha Kitambuli mkazi wa Wilaya ya Tunduru alisema kuwa
binafsi anapenda Muungano uendelee kuwapo akieleza kuwa una faida nyingi
na kwamba wanaopenda uvunjike ni waroho wa madaraka na wabinafsi,
akataka waache kuvuruga Muungano.
Aliongeza kuwa, Muungano uendelee kwani ndiyo umetufikisha tulipo na
kwamba hapendi uvunjike bali kero zilizopo zirekebishwe ikiwa ni pamoja
na Watanzania Bara wawapo Zanzibar kupewa uhuru wa kufanya biashara
kama ilivyo kwa Wazanzibari.
Naye Anispheta Malingali, mkazi wa Songea alisema Muungano uvunjwe
akidai kuwa hauna faida kwa Watanzania Bara, aliosema wamekuwa
wakinyenyekea Wazanzibar bila mafanikio na wenzao bado hawatambui
mchango wa Muungano huo zaidi ya kulalamika kila kukicha.
“Mimi binafsi naona bora tuuvunje huo Muungano, sioni faida yake kwani
wenzetu ndiyo wanafaidi kutoka kwetu. Sisi hatuna hata raha ya Muungano,
kila kukicha wenzetu wanadai huduma muhimu kama afya, maji na umeme na
wanatekelezewa, lakini bado hawaoni faida, wamepewa hadi Bunge lao bado
hawajaridhika, wamepewa Serikali bado hawaridhiki. Binafsi sioni haja ya
kuendelea kuungana na watu walalamishi wanaopenda machafuko,”alisema
Malingali.
Mtwara
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Stella Maris, mkoani Mtwara, Dk Aidan
Msafiri, alisema kuwa dhana ya Muungano ni nzuri kwani umoja ni nguvu na
Muungano ni kama mwili wa binadamu. Kikubwa ni kuzingatia maadili ya
kuungana ni lazima wote walioungana kushirikiana, kuwe na uwazi, haki
na usawa.
Yaani walioungana wawe kama wanandoa, pia kuwe na faida kwa wote
walioungana na tujifunze kwa wenzetu walioungana mfano Marekani.
Alisema kwamba kusiwe na ubabe wa kulazimisha serikali mbili au tatu,
lakini ni vyema tukarudi kwenye serikali moja. Kuwa na serikali mbili au
tatu kutakuwa na changamoto kubwa, tuwe kitu kimoja.
Naye Katibu Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Faidika Wote Pamoja (Fawopa)
la mkoani Mtwara, Komba Baltazary alisema: “Muungano una faida kubwa
kwani tumechanganya nguvu za Wabara na Wazanzibari, hivyo kuwe na mfumo
bora wa uchumi.”
Aliongeza katika muundo kwa maana ya kubakia kwa Tanganyika na Zanzibar kuwe na utambulisho kwa kila nchi kati ya nchi hizo.
“Tuwe na muundo unaoweza kujadiliwa na wananchi wote kama yalivyotolewa maoni kwenye Tume ya Katiba,”alisema.
Bukoba
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Saidia Wazee Karagwe (Sawaka) Clement
Nsherenguzi, alisema: “Ni muhimu kuonyesha kuwa tumeungana kweli kwa
kuwa na taifa moja la Watanzania na kuondoa ubaguzi unaojionyesha katika
masuala mbalimbali ikiwamo matukio yanayohusisha viongozi wa kitaifa.”
Naye Katibu wa Chama cha Walemavu, Manispaa ya Bukoba, Sweetbert Mshanga
alisema: “Muungano kati ya nchi hizo umesaidia kujenga amani na
mshikamano pamoja na kuwa ni wananchi wanaofahamu matunda ya moja kwa
moja yanayotokana na Muungano huo.”
Alibainisha kuwa faida za kuungana ni kubwa ikilinganishwa na hasara
ambayo ingepatikana kwa kutoungana, huku akitaka wananchi waelezwe wazi
faida na matunda ya Muungano.
Akitoa maoni yake kuhusu miaka hamsini ya Muungano, Mwenyekiti wa
Serikali ya Kitongoji cha Kajure katika Kisiwa cha Bumbire, wilayani
Muleba, Deogratias Mutebwa alisema kuwa ni makosa kutaka kuua Muungano
kwa visingizio vya kero zilizopo alizosema zinaweza kufanyiwa kazi bila
kuvunja Muungano na kuwa muundo unaofaa ni serikali mbili.
Mara
Damiani Thobias ambaye ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la
Sederec, wilayani Serengeti alisema kwamba Muungano haufai kuendelea
kukumbatiwa kwa kuwa hauna tija kwa wananchi.
“Kuna upungufu katika muundo wa serikali mbili, ndiyo maana wananchi
wakatoa maoni ya muundo wa serikali tatu unaolenga kutatua kero hizo,
kama unajengwa na nchi mbili, iweje nchi moja isionekane?”alihoji.
Nashoni Mkondya Mwenyekiti wa Mtaa wa Bomani mjini Mugumu (CUF)alisema:
“Wajumbe wa Bunge la Katiba wanahoji uhalali wa maoni ya waliotaka
serikali tatu, mbona hawahoji uhalali wa Rais Kikwete aliyechaguliwa na
watu wachache kuwa Rais kati ya Watanzania waliopo na wao mbona ni
wachache kuliko walioko nje lakini wanajiona halali.
Aidha, aliomba wajumbe watambue kuwa kujadili sera ya chama ya serikali
mbili wakaacha maoni ya wananchi ni kutokujua nini wanafanya kwa kuwa
Katiba ni juu ya vyama na ndiyo inaweka vyama lakini sera ya vyama
haviweki katiba.
Iringa
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), mkoani Iringa, Gotrib
Mgaya, alieleza kushangazwa na mjadala wa Bunge la Katiba unaoendelea
kwa sasa na kusema wanaopendekeza serikali mbili wanapaswa kuja na hoja
ya kuitaka Zanzibar ibadilishe Katiba yake ya mwaka 2010.
“Kwa maoni yangu Rasimu ya Pili ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji
Joseph Warioba imebeba maoni ya wananchi na ushahidi upo wa kutosha
licha ya wabunge kuupinga. Mimi nadhani muundo huo unatibu matatizo ya
muda mrefu ya Muungano,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Muundo huu ulizingatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya 2010 ambayo
imetamka kuwa Zanzibar ni nchi na kumpa mamlaka Rais wake kuwa na uwezo
wa kuunda vikosi vya ulinzi, hatua hiyo imepunguza nguvu kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Pwani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mariam Halfani, Bosco Mfundo, Amina
Hussein, Mwantumu Shaaban, Jesca Laizer, George Bundi na Machapula
Donard walisema katika miaka 50 ya Muungano udhaifu uliojitokeza
ufanyiwe kazi.
Walisema endapo pande zote zitaridhiana na kukubali kufanyika
marekebisho itawezesha kupata suluhisho la kudumu na kuondoa
manung’uniko ya wananchi wa nchi washirika za Tanganyika na Zanzibar.
Naye George Bundi alisema: “Mimi nafurahi miaka 50 sote tunasherehekea
Muungano, lakini zipo changamoto kila siku zinaelezwa kuhusu huu
Muungano, sasa basi wakati huu zifanyiwe marekebisho ili upande mmoja
usiwe na manung’uniko. Sasa kwa nini wanakataa wazi Tanganyika siyo
nchi? Wakisema hivyo basi hata huo Muungano uliopo ambao ni wa pande
mbili za nchi ya Tanganyika na Zanzibar nao haupo.”
No comments:
Post a Comment