WAZIRI
mkuu mmoja wa zamani na mawaziri wawili walioko madarakani, wametajwa
kuwa miongoni mwa wazito walioko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
walioomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Aidha, mawaziri hao wanasubiri muda muafaka ufike waweze kutangaza rasmi
kujiunga na chama hicho, kutokana na kile kilichodaiwa kuchoshwa na
mwenendo mzima wa uongozi na utendaji wa mambo unavyokwenda serikalini
na ndani ya CCM, hususan suala la kuwalinda watu wanaotuhumiwa kwa
ubadhilifu.
Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbelss Lema (pichani) aliwataja
‘wazito’ hao, kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika mjini
Sengerema juzi, ambapo alisema hatua hiyo ni ishara wazi ya kuanguka kwa
chama hicho.
Katika mkutano huo, uliofanyika katika viwanja vya Mnadani
vilivyobatizwa jina la Uwanja wa Wenje, Lema pamoja na mbunge wa
Nyamagana, Wenje walisema wananchi wengi wakiwemo baadhi ya viongozi
wenye uchungu na taifa hili ndani ya CCM, hawafurahishwi na ubadhilifu
wa mali za nchi, na kwamba hatua hiyo imewadidimiza Watanzania katika
lindi kubwa la umasikini, kutokana na kubariki madini, wanyama, misitu,
samaki na rasilimali nyinginezo kuuzwa nje ya nchi kwa maslahi ya vigogo
wachache.
Katika mkutano huo ambao zaidi ya wanachama 100 wa CCM walijiunga na
CHADEMA, wabunge hao waliishambulia serikali wakidai imekuwa kinara wa
ombaomba duniani, wakati taifa lina rasilimali nyingi zinazotumiwa na
wachache kufanya ziara za mara kwa mara ughaibuni.
Lema aliuambia umati huo wa watu kuwa kama walivyoamua kuchukua maamuzi
mawaziri hao, nao wanatakiwa kuihukumu sasa CCM na serikali yake kwa
kujiunga na CHADEMA, kwani kufanya hivyo ni kujiandaa na kile
alichokisema ukombozi wa taifa mwaka 2015.
“CHADEMA tumejiandaa kuingia madarakani kwa kutumia nguvu ya umma. Ndiyo
maana (akawataja mawaziri) wameomba kujiunga na CHADEMA ili
tulisongeshe pamoja kwenda kuingia madarakani mwaka 2015.
“Lakini (akamtaja waziri mwingine) tumemkataa. Tunataka wachapa kazi na
wenye mioyo ya kweli katika mapambano ya kupigania haki na kuondoa
dhuluma kwa Watanzania,” alisema Lema.
Awali, aliyekuwa Diwani wa CCM Kata ya Nyampulukano, Hamisi Mwagao
Tabasamu, ambaye hivi karibuni alihamia CHADEMA, aliwaambia wananchi hao
wa Sengerema kwamba, halmashauri ya wilaya hiyo imegubikwa na tuhuma za
ufisadi, hivyo viongozi wawili waandamizi wanastahili kushtakiwa
mahakamani.
“Halmashauri hii ya Sengerema kuna ufisadi mkubwa. Kuna fedha nyingi
sana za miradi zimeliwa na ushahidi ninao, TAKUKURU kama mpo hapa na
Usalama wa Taifa njooni mnikamate Jumatatu kama mnadhani ni uongo,”
alisema Tabasamu ambaye anadaiwa kuivuruga kabisa CCM wilayani
Sengerema.
Alisema, anao ushahidi wa mamilioni ya fedha za miradi katika eneo la
Bukala, zinazodaiwa kutafunwa kwa mgongo wa mafunzo jijini Mwanza, na
kwamba wananchi wa Sengerema waanze kubadilika na kuikataa CCM kwani
viongozi wake hawawasaidii katika kutatua kero zao za maji, afya,
barabara na miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Wenje aliwataka wananchi wa Sengerema kuhakikisha
wanaanza kuikataa CCM mapema, kwani bila kufanya hivyo miaka michache
watakuwa watumwa wa kupelekwa Ughaibuni kulima mashamba ya wakoloni.
“Wananchi wa Sengerema nawaambieni leo kwamba, viongozi wenu wa serikali
wanauza kila kitu sasa. Twiga wanauzwa, tembo wanauzwa, misitu, madini
navyo vinapigwa mnada kwa Wazungu,” alisema.
Alisema, ufisadi, kukumbatia wawekezaji wa nje pamoja na mikataba mibovu
ndiyo inayoiweka Tanzania katika hali ya umasikini kiasi kikubwa, huku
akimtaja mbunge mmoja wa CCM (jina linahifadhiwa), kwamba amepata
utajiri mkubwa kuliko wa marais wawili wa zamani, Baba wa Taifa, hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali
Hassan Mwinyi.
Aliwaomba wananchi hao kushinikiza katiba mpya ijayo Tanzania iongozwe
kwa mfumo wa majimbo kama ilivyo huko Bara la Ulaya, kwa madai kuwa
utarudisha mamlaka na utawala kwa wananchi, kuliko ilivyo sasa ambapo
viongozi wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wanawajibika kwa
rais
No comments:
Post a Comment