Huyu ni mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana nguvu za kutosha na
tulishangaa baada ya kutoa kete 20 kwa mara moja katika awamu ya kwanza,
jambo hili si rahisi kutokana na umri wake,”.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Bibi mmoja raia wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65)
amevunja rekodi ya umri wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Cole alikamatwa Jumatatu akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini
zilizokuwa zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara,
ambazo si rahisi kuonekana katika mitambo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana
na Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa zimesema pamoja na mbinu zake na
kujiamini, mwanamke huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa vitengo
mbalimbali vya uwanja wa ndege.
Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema mwanamke
huyo alikamatwa Mei 19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda
Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Selemani alisema raia huyo aliwasili nchini Mei 15, mwaka huu na alikaa
muda wote bila ya kuwa na shughuli yoyote, jambo ambalo lilitiliwa shaka
na kumkamata.
“Huyu mwanamke achana naye, akisimama mbele yako huwezi ukaamini kwa
jinsi anavyojiamini. Alikuwa na mbinu mpya ya kufunga hizo kete. Kila
moja ilifungwa kwa karatasi inayofanana na ganda la sigara,” alisema
Selemani.
Alisema mwanamke huyo alitumia mbinu hiyo ili asigundulike wakati akikaguliwa kwa mitambo maalumu inayogundua dawa za kulevya.
Taarifa zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake ya ufungaji wa kete,
mwanamke huyo alikuwa tayari amevuka hatua ya kwanza ya ukaguzi.
Nzowa alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
“Wakati tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha Kuthibiti Dawa za Kulevya
kilibaini na kugundua kuwa alikuwa amemeza dawa za kulevya.
“Huyu ni mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana nguvu za kutosha na
tulishangaa baada ya kutoa kete 20 kwa mara moja katika awamu ya kwanza,
jambo hili si rahisi kutokana na umri wake,” alisema Nzowa.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Nzowa alisema kikosi chake kimejipanga kukabiliana na mbinu zote zinazobuniwa na wanaosafirisha dawa za kulevya.
Takwimu za kitengo cha dawa za kulevya cha polisi zinaonyesha kuwa kati
ya Januari na Aprili mwaka huu, Cole ni mtu wa 26 kukamatwa katika
uwanja huo na raia wa tano wa kigeni kukamatwa na dawa hizo.
Raia wa kigeni wengine waliokamatwa kutoka nje ya nchi ni kutoka Marekani, Ugiriki, Kenya na Liberia na kesi zao zinaendelea.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment