Rashid Mvungi akimuangalia mtoto wake Nasrah Rashid (4) ambaye ni
mlemavu wa viungo aliyefungiwa chumbani na kufichwa kwenye boksi bila ya
kufanyiwa usafi tangu akiwa na umri wa miezi tisa. Picha na Hamida
Shariff
Morogoro. Zimeibuka
taarifa kwamba mtoto aliyekuwa amefungiwa kwenye boksi kwa miaka minne
na mama yake mkubwa, Nasra Rashid (4) alikuwa na kaka aliyefahamika kwa
jina la Nasoro ambaye hadi sasa hajulikani mahali halipo.
Wakati polisi ikisema imefurahi kupata taarifa hizo na kwamba
itazifanyia kazi, habari zilizopatikana jana kuhusu hali ya Nasra
zimesema atafanyiwa vipimo 18 ili kubaini hali ya afya yake. Vipimo vya
awali, vimebaini kuwa amevunjika mifupa ya mikono na miguu na kwamba
atapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Kuhusu kaka yake, baadhi ya majirani wa nyumba aliyokuwa anaishi mama
mzazi wa Nasra enzi za uhai wake walidai kuwa Mariamu alikabidhiwa
watoto wawili kuwalea baada ya mama yao kufariki dunia.
Mmoja wa majirani hao, Ramadhani Mansuri alisema wakati mama mzazi wa
Nasra akiishi eneo la Mjimpya alikuwa na watoto wawili akiwamo Nasoro
ambaye aliachwa akiwa na umri kati ya miaka 14-15.
Vipimo
Ofisa Ustawi wa Jamii, Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu alisema
taarifa alizopata kutoka kwa madaktari zinasema kuwa mtoto huyo
atafanyiwa vipimo 18 ili kubaini hali ya afya yake.
Akizungumzia matokeo ya vipimo vya awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali
ya Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alisema haijafahamika sababu za
kuvunjika kwa mifupa hiyo.
Dk Lyamuya alisema jana kwamba, mtoto huyo ameshafanyiwa vipimo vingine
kadhaa ambavyo vinaonyesha kwamba anasumbuliwa na homa ya mapafu
(pneumonia) na utapiamlo unatokana na kukosa lishe bora.
“Tulilazimika kumfanyia vipimo hivyo vya awali kwa sababu alikuwa
anaonekana kama anayeugulia maumivu, kwa hiyo vipimo vingine vitaendelea
kufanywa kadri tutakavyoona inahitajika,” alisema Dk Lyamuya.
Alisema kipimo cha X- Ray ndicho kilichoonyesha kuvunjika kwa mifupa
yake ya miguu na mikono na kwamba hali hiyo ndiyo inayosababisha
ashindwe kusimama na kutembea.
“Wakati anafikishwa hapa hospitalini alikuwa amebanwa na kifua na
alikuwa anashindwa kupumua vizuri. Ilitulazimu kumwekea mashine ya
oksijeni ili imsaidie kupumua, lakini sasa hali yake inaendelea vizuri
na tayari tumeondoa mashine, anaendelea na matibabu mengine,” alisema.
Mbali na tiba, Nasra pia alifanyiwa usafi wa mwili wake ambao ulikuwa
mchafu kutokana na kutoogeshwa kwa muda mrefu na sasa inaelezwa kuwa
yuko kwenye hali ya kuridhisha na wasamaria wema wameanza kujitokeza
kumpa misaada ya nguo na chakula.
Mjomba wa Nasra
Akizungumzia tukio hilo, Kaka wa Mariam, Mohamed Said alisema baada ya
dada yake kufariki dunia, Nasra alianza kulelewa na mama yake mkubwa
kutokana na baba yake mzazi kushindwa kutoa ushirikiano.
“Mimi hali yangu ya maisha ni ngumu sana nisingeweza kumlea Nasra kwa
hiyo dada (Mariamu), aliamua kumchukua amlee na naamini alikuwa
akimhudumia kwa kumpa chakula na mahitaji mengine, lakini cha kushangaza
juzi napata taarifa kuwa amekamatwa kwa kosa la kumfanyia vitendo vya
kikatili mtoto Nasra,” alisema Said.
Said alisema mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito mdogo na afya yake
ilianza kudhoofika wakati mama yake alipokuwa mgonjwa na baada ya
kufariki dunia, viungo vya Nasra vilionekana kulegea na kushindwa
kutembea na kusimama.
“Kabla ya kifo cha mama yake, Nasra aliumwa sana, lakini dada Mariamu
alimlea vizuri na baada ya kugundua kuwa na ulemavu alijitahidi
kumfanyisha mazoezi ya kumsimamisha lakini mtoto mwenyewe alikuwa
anagoma, alipolazimishwa alikuwa analia sana, hivyo alikuwa anakaa tu
mahali pamoja na kujisaidia haja ndogo na kubwa hapohapo,” alisema Said.
Alisema taarifa kwamba Nasra alikuwa akiishi kwenye boksi na kuteswa, si
za kweli kwani licha ya kumlea, Nasra dada yao alishawahi kuwalea
watoto wengine wa ndugu zao bila ya kuwafanyia vitendo vya aina hiyo.
Alisema familia haitaweza tena kumlea mtoto huyo, kwani imepatwa na hofu
ya kupata lawama kama aliyoipata dada yake, hivyo wanaiachia Serikali
kumlea mtoto huyo au baba yake ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Morogoro.
Kuhusu malezi, Ngungamtitu alisema: “Tumeongea na Rashid Mvungi ambaye
ni baba mzazi wa Nasra na yeye amesema itakuwa vigumu kumchukua kwenda
kumlea kwa sababu alimzaa nje ya ndoa na hakuwahi kumwambia mke wake
mpaka tukio hilo lilivyotokea. Hatuwezi kumlazimisha.”
Uchunguzi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema uchunguzi wa
tukio hilo unaendelea na kwamba jeshi hilo limefunga chumba cha
mtuhumiwa kwa ajili ya usalama na kuepuka kuharibika kwa ushahidi wa
mazingira.
Alisema jeshi lake litashirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii
kuhakikisha kuwa Nasra anakuwa salama hospitalini na kwingineko
atakakopelekwa kwa sababu mbalimbali.
REJEA
Nasra aligundulika akiwa
amewekwa katika boksi nyumbani kwa mama yake mkubwa, Mariamu Said,
mkazi wa Kiwanja cha Ndege, Morogoro aliyekuwa akimlea. Hivi sasa,
Mariam pamoja na mumewe, Omar Mtonga wanashikiliwa na polisi kwa
kumficha mtoto wa huyo kwenye boksi kwa miaka minne.
IJIMAMBO

No comments:
Post a Comment