Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha
majumuisho ya ziara
yake ya mkoa wa Arusha kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha,
Desemaba 18, 2016. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho
Gambo.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda tume kuchunguza taarifa
inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya
Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi
ya Grumeti Serengeti pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo.
Amesema
timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumet kwa ajili
ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya faru John na
kisha watakwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya
watoto wake na kuvilinganisha na pembe hiyo ili kubaini kama kweli
pembe aliyopelekewa ni ya faru John au laa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Desemba 18, 2016) wakati wa majumuisho ya
ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga kukagua
utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa
wananchi.
"Tume
niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumet
Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo
wachukue vinasaba na baada ya hapo watakwenda Creter na kuchukua
vinasaba vya watoto wa faru John na kuvipima kwa pamoja. Lengo ni kutaka
kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya
faru John,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema wakati faru John akiwa V I P Grumet taarifa zilisema ni
mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza akabaini faru huyo hakuna
na ugonjwa wowote.”Daktari alimpima tena kwa mara ya pili taarifa
zikasema tena si mgonjwa ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani,”.
Waziri
Mkuu amesema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa
hizo kikamilifu kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru
hao kutoka nchini Afrika Kusini. Ni lazima nyara hizo za Serikali
zilindwe kwa manufaa Taifa.
Waziri
Mkuu alipokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru
John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary
iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Desemba 9, 2016 katika kikao
kilichofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es
Salaam.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Baada ya kupokea taarifa
hiyo Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa
ofisi yake.
Akisoma
taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia
Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na
asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Kati
ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na
asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha
kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya
Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.
Baada
ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya
faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu.
Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru.
Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa
TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi
pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa
Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande
alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6
na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Desemba
6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza
uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote
zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye
hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.
Alitoa
agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani
Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo
pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya
kikazi mkoani humo.
No comments:
Post a Comment