MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, anakusudia kumshitaki Waziri wa Maji,
Profesa Jumanne Maghembe, kwa madai ya kumnyima nyaraka zinazohusiana na
miradi ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mnyika amesema kuwa anataka mahakama imlazimishe Waziri Maghembe, azitoe
nyaraka hizo ili mbunge huyo azifanyie kazi anayokusudia.
Akizungumza na Tanzania Daima, wakili wa Mnyika, John Mallya, alisema
amepokea maelekezo kutoka kwa mbunge huyo kufungua kesi hiyo.
Alibainisha kuwa Mnyika anataka nyaraka hizo zimsaidie kuwakilisha wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali.
Kwa mujibu wa wakili, wengine watakaojumuishwa katika kesi hiyo ni
pamoja na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Fredrick Werema.
Wakili Mallya, alisema mteja wake aliomba nyaraka hizo na kwa mujibu wa
kifungu cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge,
alishafuata taratibu zote husika, lakini Waziri Maghembe hakumpa nyaraka
hizo.
Mallya, alisema Mnyika alishamuandikia barua Prof. Maghembe, kuomba
nyaraka hizo tangu Januari 3 mwaka 2013 kisha kumkumbusha tena Mei mwaka
huu, lakini hatoi majibu.
Mnyika pia anataka mikataba yote ya maji inayotekelezwa katika jimbo la
Ubungo ikiwa pamoja na fedha za mikopo ya ndani na nje pamoja na ripoti
za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali za mwaka 2010 hadi 2013,
zilizokaguliwa.
Januari mwaka huu, mbunge huyo alimtaka Prof. Maghembe ajiuzulu kutokana
na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam
kinyume na maelezo yake aliyoyatoa bungeni Februari 4 mwaka jana.
CREDIT:MTANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment