Tangu kuanza kwa ugonjwa huo Januari mwaka huu hadi kufikia juzi jumla
ya wananchi 494 wa mkoani hapa walipimwa na kugundulika kuwa na vimelea
vya homa hiyo, kati yao akiwamo Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili
nchini, Gilbert Buberwa wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu fungu hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki alisema mkoa ni hapa halmashauri imetenga jumla ya Sh218 milioni
zinazotumika kwa sasa katika kupambana na ugonjwa huo.
“Fedha hizo zinatumika kwa sasa katika kutoa huduma mbalimbali za
dharura kwa wananchi wa mkoa huu kutokana na homa hiyo wakati
tukiendelea kutafuta vyanzo vingine ili kuongeza kasi ya mapambano
haya,” alisema Sadiki.
Mkuu huyo alifafanua kuwa katika fedha hizo kila manispaa itatumia kiasi
chake na Manispaa ya Temeke itatumia kiasi cha Sh24 milioni, Ilala Sh32
milioni na Kinondoni Sh150 milioni.
“Tayari manispaa hizo zimeanza kufanyia kazi fedha hizo kwa kuendesha
shughuli mbalimbali za kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo husika, ikiwamo
elimu ya usafi ambayo ndiyo msingi wa kuepukana na ugonjwa huu,” alisema
Sadiki na kuongeza pia watanunua vifaa vya kupimia wagonjwa (Test kits)
vitakavyokuwa vinatumika katika hospitali za manispaa hizo.
Hata hivyo Sadiki alisema hatua hizo ni za mwanzo na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kupambana na ugonjwa wa dengue.
Akizungumzia Sh500 milioni zilizoahidiwa bungeni mapema wiki hii na
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe, Sadiki
alisema fedha hizo bado zinashughulikiwa na mfuko wa Hazina na pindi
zitakapotoka basi zitaongeza nguvu katika mchakato wa kupambana na homa
hiyo nchini.
Sadiki alisema mbali na hatua hiyo zoezi la kuweka viua vijidudu kwenye
maji yaliyotuama ili kuwaangamiza viluilui wa mbu linaendelea, hadi sasa
jumla ya kata 58 zinaendelea kuweka viuadudu na kuharibu mazalia ya
mbu.
Mkuu huyo alisema kuwa zoezi la kunyunyiza dawa litafanywa nao kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra)
kwenye magari 600 yanayofanya safari zake kati ya Dar es salaam na
mikoani.
mwananchi.
No comments:
Post a Comment