Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe akisoma hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha
2014/15, bungeni mjini Dodoma juzi. Viti vya wabunge wa Kambi ya
Upinzani vikiwa wazi baada ya wabunge hao kususa na kutoka nje kutokana
na kukasirishwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Federick
Werema aliyoitoa bungeni. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma/Dar es Salaam. Kashfa ya zaidi ya Sh200 bilioni za Akaunti ya
Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua sura mpya baada ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kudai kuwapo kwa
watu wanaonunua mashahidi.
Jaji Werema alitoa kauli hiyo nzito bungeni mjini Dodoma juzi, kauli
ambayo imeibua maswali mengi kuliko majibu, kuhusu ni nani wanaotoa
fedha kutafuta mashahidi na kwa masilahi ya nani hasa.
“Ninafahamu kwamba kuna watu wengi wanatumia fedha kwa ajili ya kutafuta
mashahidi, lakini haituhusu, palipo na haki, haki itasimama na haki ya
mtu haipotei,” alisema Werema katika kauli inayoonyesha kukata tamaa.
Werema alitoa wito kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuendelea
na uchunguzi na waufanye haraka na kwa umakini.
“Uamuzi uliofanyika hapa ni kwamba uchunguzi uendelee na vyombo
vilivyoteuliwa ni Takukuru na CAG na bado vinafanya uchunguzi… Nahimiza
vyombo hivyo vifanye kazi hiyo haraka na kwa umakini,” alisema.
Hata hivyo, Werema alitahadharisha kuwa ni vyema ikafahamika, akaunti ya
Escrow ilianzishwa kwa malengo maalumu. Akaunti hiyo ilifunguliwa na
Kampuni ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Werema alikiri zipo kodi ikiwamo ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambayo
ilipaswa kulipwa na Tanesco na kodi ya Manufaa (capital gain) inapaswa
kulipwa na Kampuni iliyoiuza IPTL kwa Pan African Power Ltd (PAP).
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hoja iliyopo na
inayoleta ubishani ni kuondoa fedha katika akaunti ya Escrow na
kuzipeleka.
Waziri Mkuu alisema: “Kwa tuhuma zenyewe zilivyo itabidi tuwahusishe
Takukuru nao wafanye kazi kwa upande wao ili kupata ukweli kwa sababu
wako pia viongozi wa Serikali wanaotuhumiwa katika suala hilo, hivyo ni
vyema likachunguzwa kwa uzito wake ili wale watakaobainika wamekula
rushwa washtakiwe.
Kadhalika Waziri Mkuu aliliomba Bunge limruhusu CAG kukamilisha kazi hiyo.
Lema
Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, jana
alihoji Serikali inatoa wapi nguvu na sauti ya kukemea rushwa katika
taasisi zake wakati baadhi ya viongozi wanadaiwa kuhusika na kashfa ya
IPTL.
“Kama wanaopaswa kukemea na kuzuia rushwa ni wala rushwa, ni wazi moja
kwa moja kuwa utamaduni wa kupokea rushwa katika taasisi zote za
Serikali ni jambo la kawaida na linaloipendeza Serikali ya CCM,”
alisema.
Lema alitoa shutuma hizo wakati akisoma hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara
hiyo kwa mwaka 2014/15.
Lema alienda mbali zaidi na kudai: “Hakuna kiongozi hata mmoja mwenye
mamlaka ya kiuadilifu kukemea jambo hili kwa kuwa familia zao zinaishi,
zinasoma na kufurahia maisha kwa ajili ya ufisadi”.
Alidai kuwa viongozi wa Serikali ndiyo vinara wa migogoro na uuzwaji wa dawa za kulevya nchini.
Shutuma nyingine ambayo Lema aliitoa ni kuhusu uchochezi wa masuala ya
udini na ukabila katika taifa na kusema kwamba yanasababishwa na uzembe
unaofanywa na viongozi wa Serikali ya CCM.
Mbunge huyo alisema kuwa baadhi ya vigogo serikalini wamekuwa ndiyo
vinara wanaofanya biashara ya dawa za kulevya, lakini bado hawajakamatwa
wala kutajwa hadharani kama ambavyo serikali imekuwa ikiahidi mara
zote.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina sababu za kupoteza muda katika
eneo hili, kwani ni ukweli usiopingika kuwa biashara hii inafanywa na
viongozi wakuu wa Serikali, hivyo basi waamue wao wenyewe kama
wangependa kuendelea kuwa sehemu ya mateso na mauaji ya vijana wetu
katika jamii ya watu inaowaongoza,” alisema Lema.
Alihalalisha kauli yake kuwa, katika nyakati tofauti, Rais Jakaya
Kikwete alishatangaza hadharani kwamba anawajua kwa majina vigogo
wanaojihusisha na dawa za kulevya, lakini inashangaza akiwa Amiri Jeshi
Mkuu ameshindwa kuwataja kwa majina watu hao.
“Rais wa nchi ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama anaogopa kuwataja wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa majina
ambao alisema anawajua, je, tushawishike kuwa watu hao ambao hata Rais
aliwagwaya ni Malaika au ni Mungu?” Alihoji Lema.
Alisema kumekuwa na uzembe mkubwa ambao unafanywa na polisi kwa
maelekezo ya viongozi wa CCM waliopo madarakani kiasi cha kuwaachia
watuhumiwa hadharani kwa visingizio vya ajabu.
Kiongozi huyo alitolea mfano wa watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa
kiongozi wa Chadema wa Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo ambaye
alichinjwa na wauaji walikamatwa lakini wakatorokea mikononi mwa polisi.
“Wauaji wale walikamatwa na Polisi lakini cha kushangaza waliweza
kutoroka mbele ya Polisi kwenye chumba cha mahakama wakiwa na pingu
pamoja na kumpora askari bunduki.”
Mdee
Katika mchango wake bungeni, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alimlipua
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa kile alichodai kukumbatia
majalada ya rushwa kubwa kwa masilahi yake binafsi.
Mdee alisema DPP amekuwa akilalamikiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kwamba amekuwa
kikwazo katika kushughulikia kesi kubwa za rushwa.
“Juzi tunaambiwa hapa suala la akaunti ya Escrow, Sh200 milioni
mnapeleka Takukuru na kwa CAG… Sheria ya mwaka 2007 iko wazi kwamba
hairuhusiwi kuwataja wala rushwa wakubwa na mafisadi kwa majina,”
alisema.
“Akitaka kufungua shauri la rushwa kubwa kubwa (Dk Hosea) mpaka akaombe
kibali kwa DPP… Analalamika DPP amekuwa akibania vibali vya kufungua
kesi kwa masilahi yake binafsi,” aliongeza kusema Mdee.
Hosea azungumza
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea alisema kuwa mashtaka hayo
404 ni ya mwaka wa fedha unaoishia Juni.
Alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi ipasavyo ndio maana walifanikiwa
kuwasilisha kesi hizo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Eliezer Feleshi
kwa ajili ya hatua zaidi.
Alipoulizwa kuwa ni kitu gani huchelewesha kazi zake, Hosea alisema kuwa
hakuna kinachowachelewesha kwa kuwa kuna mgawanyo wa madaraka baina ya
taasisi yake na DPP.
“Takukuru tunachunguza makosa ya rushwa na DPP anaandaa mashtaka. Hivyo
tunafanya kazi zetu kama inavyotakiwa,” alibainisha Hosea.
Kuhusu majalada 103 yaliyorudishwa Takukuru kwa uchunguzi zaidi, Hosea
alisema wanaendelea kuyafanyia kazi na kusisitiza kwamba hawezi kusita
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote ambao hati zao za mashtaka
zitakuwa zimekamilika.
Kwa nyakati tofauti kumekuwa na tuhuma kuwa baadhi ya kesi za rushwa hupigwa danadana makusudi kwa kuwa zinahusisha vigogo.
DPP asema anasingiziwa
Hata hivyo, DPP Feleshi alisema kuwa mambo ambayo huzungumzwa ni
nadharia na kwamba wanaotuhumu kuwa taasisi yake inawabeba vigogo
hushindwa kutoa vithibitisho.
“Hao watu wanaosema kuwa nawabeba vigogo wataje hizo kesi ni zipi? Na
kila siku wamekuwa wakisema hayo mambo lakini ukiwaambia waseme huwa
wanatokomea, hakuna aliyewahi kutaja,” alisisitiza Feleshi na kuongeza:
“Mimi siwezi kuchelewesha makusudi majalada ya watu kwa sababu ni
vigogo, hiyo si kazi yangu. Ufanisi wangu ni kuhakikisha majalada yote
yanayoifikia ofisi yangu yanafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.”
Imeandikwa na Daniel Mjema, Habel Chidawali, Dodoma, Nuzulack Dausen, Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment