SERIKALI
imesema itaendelea kutoa dawa zinazotibu sumu ya nyoka ili kupambana na
tatizo hilo nchini. Kauli hiyo ya serikali ilitolewa Dar es Salaam jana
na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu.
“Kama
tunavyofahamu nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi
wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu
kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa
wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.”
Alisema
dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi; na kwamba si
tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa.
Waziri
huyo alisema bei ya kununulia dawa hizo ni kati ya dola za Marekani 55
hadi 85 (yaani Sh 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo kimoja.
Alisema
kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu baada
ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja
tu.
Waziri
alisema pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) kila mwaka huagiza dawa hizo kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu
wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni Sh
200,000 kwa kichupa kimoja.
“Hospitali
zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa
wasambazaji wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika
wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika. “Napenda
kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za
tiba hutolewa bure kwa makundi maalumu au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya
gharama, au kwa kupitia mfumo wa bima mbalimbali za afya kama vile CHF.
“Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika,” alisema Waziri.
Alisema
katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka
wanahudumiwa ipasavyo, waganga wakuu wa mikoa na viongozi wa hospitali
zote nchini, wanatakiwa kuhakikisha hospitali zote za umma zinaingiza
dawa hiyo katika dawa za dharura ili iweze kununuliwa kama dawa zingine
za dharura kupitia kifungu cha fedha za dawa za dharura.
Alisema kwa wagonjwa ambao watakuwa na bima ya afya, gharama za matibabu hayo zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa bima.
“Wananchi
wanahimizwa kujiunga na Bima za Afya (CHF/ NHIF) ili kupata unafuu wa
matibabu haya na mengine. Mfano CHF - gharama ya kujiunga katika
halmashauri mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000 hadi shilingi
30,000 kwa mwaka.
“Kwa
wagonjwa ambao watakuwa hawana bima ya afya, watatakiwa kuchangia
gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango
kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri
itakavyohitajika.
“Hii
ni kutokana na ukweli kwamba kung’atwa na nyoka ni ajali na wananchi
wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi
uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya
nyoka ni mdogo,” alisema Waziri Ummy.
Alisema
wagonjwa watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo,
hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za
afya, wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa
msamaha wa gharama hizo.
No comments:
Post a Comment