(Picha zote na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
Na Immaculate Makilika –MAELEZO_DAR ES SALAAM
WAZEE
wa Mkoa wa Dar es salaam wamewaomba Umoja wa Katiba wa Wananchi (UKAWA)
kurudi Bungeni ili kuendelea na mchakato wa majadiliano ya Rasimu ya
Katiba Mpya yanayoendelea.
Wazee
hao wamesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wakizungumza na
waandishi wa habari kuhusu hali ya siasa nchini pamoja na Bunge la
Katiba Mpya linaloendelea mjini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Wazee wenzake Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamedi Ligora , amesema kuwa Tanzania
ni nchi nzuri na watu wake ni wazuri ni vema UKAWA na wenzao wakarudi
Bungeni kujadiliana ili watimize matakwa ya kidemokrasia.
Amesema
kuwa wananchi wa Tanzania hawataki kufananishwa na nchi zingine
zilizofanya makosa na kupata matatizo kutokana na mambo kama haya ambayo
yalisababisha wananchi wao kuzikimbia nchi zao kwa mambo ambayo
wangeweza kukaa chini na kumaliza wenyewe kwa ajili ya maslahi ya umma.
Kapteni
Mstaafu Alhaji Ligora amesema kuwa suala la mchakato ni suala la
kidemokrasia, hivyo ni vyema UKAWA wakatumia fursa hiyo waliyonayo kwa
kurudi Bungeni na kuendelea na majadiliano kuhusu Rasimu ya Katiba hali
itakayosaidia kupatikana kwa Katiba Mpya ambayo itakuwa na manufaa kwa
wananchi wa Tanzania.
Aidha,
amewaomba wajumbe walio Bungeni na wale walio nje ya Bunge kuacha
kuwazomea UKAWA badala yake wawasihi warudi katika chombo rasmi cha
kuboresha Rasimu ya Katiba Mpya.
Naye
Mzee Ali Bakari Muki, amewataka UKAWA kuheshimu misingi ya demokrasia
lakini pia amewapongeza wabunge walioitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kurudi Bungeni na
kuendelea na majadiliano kuhusu Katiba kwani ndio Jukwaa pekee la
kuwapatia wananchi Katiba bora.
Kwa
upande wake Mzee Yahaya Ngoma amewataka viongozi wote hasa UKAWA
kuheshimu na kudumisha jitihada zilizofanywa na waasisi wa Taifa hili
akiwemo Baba
wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Sheikh Abeid Amani
Karume kwa kuzingatia misingi na kanuni za uongozi bora kwa kutumia
njia ya majadiliano pale panapokuwa na mawazo tofauti baina yao.
Halikadhalika,
Alhaji Sheikh Bakari Chikawa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia kuanza kwa mchakato
wa Katiba Mpya na kusisitiza ni moja ya tunda la uongozi bora na
demokrasia nchini.
Aidha,
ameongeza kuwa UKAWA ni vema wakatumia fursa hiyo ya demokrasia kwa
kuwawakilisha vema wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanapata Katiba
Bora.
No comments:
Post a Comment