Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe
akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu msimamo wao wa kutorudi
bungeni kujadili Rasimu ya Katiba Mpya. Wengine ni wenyeviti wenza wa
umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) na James Mbatia. Picha na
Michael Matemanga
Dar es Salaam. Joto
la Katiba Mpya linazidi kupanda nchini, huku baadhi ya wasomi na makundi
mbalimbali ya watu wakizidi kutilia shaka utapatikanaji wa Katiba hiyo.
Wakizungumza katika mdahalo uliohusu mivutano ya makundi katika mchakato
wa Katiba Mpya jana jijini Dar es Salaam, walisema kuwa CCM haikuwa na
nia njema tangu mwanzo, huku Rais Jakaya Kikwete akitajwa kushindwa
kusimamia ipasavyo.
Profesa Lumumba alisema Katiba ya Tanzania imejaa viraka na kwamba
inahitajika Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa ya Watanzania na karne
ya 21, itakayokwenda sambamba na changamoto za Afrika Mashariki.
Alisema nchi za Afrika Mashariki zilipata katiba zao kwa njia ya
machafuko, hivyo Tanzania lazima itafute njia sahihi inayokubalika kwa
wananchi wote bila ya kuwepo kwa kundi moja linalotaka kuhodhi mchakato
wa Katiba Mpya.
“Tanzania ina nafasi ya pekee na kihistoria kujipatia Katiba Mpya bila
vita na itakuwa ni jambo la kusikitisha ikiwa kwa mtazamo finyu ya
kivyama utanyimwa na wanasiasa ambao fikra zao si za kukidhi matakwa ya
katiba,” alisema Profesa Lumumba.
Alieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa alifanya makosa katika
kusimamia mchakato wa Katiba Mpya, hivyo Watanzania wanapaswa wamsamehe
ili mambo yaende sawa.
“Nimesikiliza hotuba za Rais (Jakaya Kikwete) alikubali kwamba alikosea,
tukumbuke Rais wa nchi hawezi akaja akapiga magoti, cheo chake cha rais
hakikubali hivyo, akisema alitoa maoni kama mwananchi kile ambacho
anasema ni kwamba nisameheni,” alisema huku akishangiliwa na wajumbe
ukumbini. Aliongeza kuwa iwapo Watanzania watataka Rais afanye jambo la
ziada kuliko hilo alilofanya watashusha hadhi ya kiongozi huyo wa nchi.
Alisema Watanzania walipotunga sheria ya kufanya marekebisho ya katiba
walifanya dhambi mbili za asili. Alizitaja dhambi hizo kuwa ni kuruhusu
kuyataja baadhi ya mambo kwenye katiba kuwa ni matakatifu na kuvunja
tume ya mabadiliko ya katiba.
“Mkiwa mnazungumzia mambo ya katiba hakuna mambo matakatifu yote lazima
yazungumziwe. Tanzania siyo nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutafuta
katiba ni nchi ya mwisho,” alisema huku akishangiliwa na wajumbe wa
kongamano hilo.
Akiizungumzia dhambi ya pili alisema: “Lakini jambo ambalo halieleweki
na wengi ni kwa nini Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba
(Joseph) iliyokuwa na uzoefu ikavunjwa ? Katika mataifa yote unaihifadhi
tume mpaka mwisho.”
Alisema tume hiyo ilitekeleza kazi yake kwa kiwango kikubwa na kwamba
hakuna nchi Afrika iliyowahi kukusanya maoni kutoka kwa kila mwananchi.
Akizungumzia namna wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba linaloanza kikao
chake cha pili Jumanne mjini Dodoma wanavyotakiwa kufanya kazi zao,
alisema siku zote mjumbe ni mtu anayepeleka taarifa mahali fulani kama
ilivyo na siyo kuibadilisha.
“Hilo ndilo jambo linalotambulika na mataifa yote na nyinyi Watanzania
ndiyo mtakuwa wa kwanza kufikiri tofauti…Tume ya Warioba imefanya mambo
yenye ubora yaliyopita viwango vya kimataifa,” alisema huku
akishangiliwa kwa makofi na miluzi.
Alisema Ukawa wamefanya vizuri kujiondoa bungeni kwa kuwa walikuwa na
sababu zinazoeleweka, lakini kwa kuwa sasa ujumbe wao umefika CCM
wanaweza kurudi bungeni.
“Kama umejiondoa pindi ujumbe wako unapoeleweka unarudi bungeni ili upambanishe hoja,” alisema.
Profesa Lumumba alisema wanachama wa TLS wanatakiwa kuchukua hatua ya
kufungua kesi mahakamani kuhoji uhalali je, katika kujadili Mamlaka ya
Bunge hilo yanaishia wapi.
Jenerali Ulimwengu
Mchambuzi mkongwe wa masuala la kisiasa nchini, Jenerali Ulimwengu
alitaja sababu zilizosababisha kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya ikiwa
ni pamoja na CCM kutokuwa na nia ya dhati ya kupata katiba hiyo.
Alisema vyama vya upinzani vilidhani vingeweza kutumia mchakato wa
Katiba Mpya kuingia Ikulu huku CCM nao wakidhani iwapo katiba
ingepatikana wangepoteza madaraka yao.
“Watawala walisema hatuhitaji mabadiliko, hasa mtawala mkuu kuliko wote
akasema tutakuwa na katiba mpya. Kwa hiyo tulikuwa mahali ambapo
watumishi hawataki tajiri anasema atafanya,” alisema Ulimwengu.
Rais Mstaafu wa TLS, Francis Stolla alisema kufungua kesi ni lazima
kuwapo na mlalamikaji lakini wataona ni jinsi gani wataweza kufungua
kesi mahakamani ili mahakama itoe ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge hilo.
Naye Mwakilishi wa Chadema, Tundu Lissu alisema mjadala kama huu
umechelewa ulitakiwa kufanyika miaka mitatu nyuma ambapo tungejiuliza
wapi tunataka kwenda na tunataka kitu gani.
Ukawa watoa msimamo
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeendelea na msimamo wao wa
kutorejea bungeni Agosti 5 mwaka huu na nguvu zao wanazielekeza katika
vyama vyao kwenda kujipanga ili kuhakikisha harakati za kupigania Katiba
Mpya zinafanyika nje ya Bunge.
Pia, Ukawa wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kuwa kigeugeu na awe na
msimamo katika jambo hili lenye masilahi mapana kwa kila mwananchi.
Kauli ya Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi
inatolewa ikiwa ni siku moja kupita baada ya kuvunjika kwa kikao cha
usuluhishi kilichokuwa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji
Francis Mutungi.
Kikao hicho kilichofanyika Hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam,
kilianza saa 4 asubuhi na kumalizika saa 1.30 usiku kwa Ukawa na CCM
kuondoka bila kuafikiana hasa uhalali wa mamlaka ya Bunge Maalumu la
Katiba ni yapi.
Jaji Mutungi akizungumza juzi na gazeti hili alisema hatima ya
Watanzania kupata Katiba Mpya itategemea busara za viongozi wa vyama vya
siasa.
“Ninavyoona mimi, hapa hatima ya Watanzania ya kupata Katiba Mpya
itategemeana na busara za viongozi wetu wa vyama vya siasa pekee na si
kitu kingine,” alisema Jaji Mutungi.
Wakizungumza jana na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya
Chadema jijini Dar es Salaam, viongozi wa Ukawa walisema hawatarejea
katika Bunge Maalumu la Katiba na wataendelea kuyaheshimu maoni ya
wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
“Ukawa hatuko tayari kuendelea na mazungumzo na CCM wala kurudi katika
mkutano wa Bunge Maalumu kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti maoni ya
wananchi na kutumia vibaya fedha za umma na kubariki uchakachuaji wa
msingi wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume,” alisema Freeman
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema.
Aliongeza: “Kila chama kinakwenda kujadili na wanachama wake kupitia
Kamati kuu zake kisha tutakutana ili kuona ni hatua gani zingine
tuzifuate katika kuipigania Katiba Mpya.”
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema hotuba ya Rais
Kikwete aliyoitoa juzi amewapotosha Watanzania na kuendelea kuuvuruga
mchakato huo kama alivyofanya wakati akilizindua Bunge Aprili mwaka huu.
“Rais Kikwete alipewa fursa na Tume ya Katiba kutoa maoni yake, lakini
alikataa sasa kule bungeni alitoa maoni ya nini wakati alitengewa muda
na akaukataa? Na juzi katika hotuba yake ameendelea kusisitiza kuwa
alitoa maoni kama mwananchi, anauharibu mchakato huu,” alisema Profesa
Lipumba.
Aliongeza: “Rais Kikwete anafanya mchezo kama ingekuwa ngoma ya kikwere
angefanya hivyo lakini kwa jambo hili la kitaifa anatakiwa kuwa makini
sana.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema katiba
mpya itapatikana kwa utashi wa kisiasa na si maridhiano. Naye Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema marekebisho
yaliyofanywa na Bunge Maalumu la Katiba Aprili 25 mwaka huu baada ya
wajumbe wa Ukawa kutoka yalikuwa ni batili.
“Mabadiliko hayo yaliingiza kanuni mpya ya 32 (6) inayoliruhusu Bunge
Maalumu kupendekeza sura mpya kwenye rasimu sasa hii hata tukirudi CCM
watataka kuibadili rasimu nzima na kuitupilia mbali Rasimu ya Tume ya
Katiba,” alisema Lissu.
No comments:
Post a Comment