WAKATI Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) awamu ya kwanza, unapanga kuongeza nauli za daladala kwa wakazi wa Dar es Salaam ili kukabiliana na tatizo sugu la foleni, taarifa ya matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara, zimeonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam, ndio mahali ghali zaidi nchini.
Gazeti
hili lilichapisha kwa mara ya kwanza habari kuwa Dart awamu ya kwanza
ikianza, nauli ya basi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam
kwenda na kurudi vituo vikubwa vikiwemo vya Kariakoo, Posta na Kimara,
itapanda kutoka nauli ya chini ya Sh 400 ya sasa mpaka Sh 700 na 800 kwa
ruti moja.
Taarifa
hiyo ya kaya, ambayo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii,
Ephraim Kwesigabo, alisema jana kuwa ni ya awali tu na taarifa yenyewe
itatolewa hivi karibuni, imeonesha kuwa mkoa huo ndio wenye gharama
kubwa ya maisha.(Martha Magessa)
“Mfano,
bei za vyakula ni kubwa jijini Dar es Salaam, ukilinganisha na maeneo ya
vijijini, hivyo gharama ya kulipia mlo wa mtu mmoja kwa siku ni ya juu
kwa jiji la Dar es Salaam,” imeeleza taarifa hiyo. Hata hivyo, taarifa
hiyo inayoangalia viashiria vya umasikini kwa kuchambua mahitaji muhimu
ya mwanadamu, iliyo katika tovuti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS),
imefafanua pia kuwa mkoa huo ndio wenye idadi ndogo ya masikini nchini.
“Kaya za
jijini Dar es Salaam zina kiwango kidogo cha umasikini wa mahitaji ya
msingi, ukilinganisha na kaya zinazoishi katika miji mingine na maeneo
ya vijijini. “Ukijumuisha watu wote wenye umaskini wa mahitaji ya msingi
nchini, inakadiriwa asilimia mbili (1.5) wanaishi jijini Dar es Salaam,
asilimia 14.4 wanaishi maeneo mengine ya mijini na asilimia 84.1
wanaishi vijijini,” alisema.
Kuhusu
umiliki wa nyumba, taarifa hiyo imeeleza kuwa wakati asilimia 76 ya kaya
nchini zinamiliki nyumba wanazoishi, jijini Dar es Salaam ni asilimia
37 tu ya kaya zinazomiliki nyumba wanazoishi na kaya zilizobakia,
asilimia 63 ni wapangaji.
“Uwiano
huu (wa nyumba za kuishi) ni mkubwa katika maeneo ya vijijini, ambako
asilimia 89 ya kaya wanamiliki nyumba wanazoishi, huku umiliki wa nyumba
katika maeneo mengine ya mijini ukiwa asilimia 58,” imeeleza taarifa
hiyo.
Taarifa
hiyo ingawa ni ya awali, lakini iliyochambua vema umasikini kwa
kuangalia mahitaji ya lazima na mahitaji muhimu ya Watanzania, imebaini
hadhi za nyumba wanazoishi Watanzania kwa ujumla imekuwa ikiboreka.
“Asilimia 66 ya kaya mwaka 2011/12 zinaishi katika nyumba zenye paa za kisasa ukilinganisha na asilimia 55 ya kaya mwaka 2007.
“Vivyo
hivyo, asilimia 73 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa kuta
imara mwaka 2011/12 ukilinganisha na asilimia 33 za mwaka 2007,”
imeeleza taarifa hiyo.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, kuta imara zinajumuisha zilizojengwa kwa mawe,
matofali ya saruji, au matofali ya kuchoma na paa za kisasa ni zile
zilizojengwa kwa mabati. Katika mawasiliano, taarifa hiyo imeeleza kuwa
umiliki wa simu za mkononi unatofautiana sana kwa maeneo.
“Wakati
kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo mengine ya mjini na asilimia 88
ya kaya za Dar es Salaam, zinamiliki angalau simu moja ya mkononi, ni
asilimia 45 tu ya kaya za maeneo ya vijijini zinazomiliki angalau simu
moja ya mkononi,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo, imeeleza kuwa mstari wa masikini, unaonesha masikini wa mahitaji
ya msingi nchini na ambaye yupo katika mstari wa umasikini wa mahitaji
yamsingi ni anayepata Sh 36,482 kwa mwezi, wakati maskini wa chakula ni
anayepata Sh 26,085 kwa mwezi.
“Kwa
kutumia takwimu hizi, matokeo yanaonesha kuwa zaidi ya robo (asilimia
28.2) ya watu wote waishio Tanzania Bara, wako chini ya mstari wa
kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi na asilimia 9.7 ya watu wote
wapo chini ya mstari wa umaskini wa chakula,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata
hivyo, taarifa hiyo imeonesha kuwa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya
msingi kwa Tanzania Bara kimekuwa kikipungua kwani mwaka 2007, kilikuwa
asilimia 33.6.
“Matokeo
ya awali yanaonesha kupungua kwa kiwango cha umaskini kati ya 2007 na
2011/12. Upimaji wa mwenendo wa umaskini utaainishwa kwenye Ripoti Kuu
ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, 2011/12,” imeeleza
taarifa hiyo.
Hesabu
zilizopigwa na wataalamu wa takwimu walioandaa taarifa hiyo,
zimebainisha kuwa kunahitajika Sh bilioni 103.3 kwa mwezi (sawa na zaidi
ya Sh trilioni 1.2 kwa mwaka), ili kuondoa umaskini wa mahitaji ya
msingi kwa watu waishio chini ya mstari wa umaskini Tanzania Bara.
Pia
imeelezwa kuwa kama watu wote wangegawanywa katika makundi matano
yanayolingana na ukubwa wa matumizi yao kuanzia wa chini hadi wa juu,
matumizi ya watu wa kundi la juu (matajiri sana) ni mara nne (4) ya
matumizi ya kundi la chini (maskini sana) kwa Tanzania Bara.
Katika
elimu, taarifa hizo zimeonesha kuwa asilimia 20 ya Watanzania (Tanzania
Bara) wenye umri wa miaka 15 au zaidi hawana elimu ambapo kwa mwaka 2007
ilikuwa ni asilimia 19.
Aidha,
uandikishwaji katika shule za msingi kwa watoto wenye umri kati ya miaka
7 hadi 13, umeshuka na kufikia asilimia 78 kwa mwaka 2011/12
ikilinganishwa na asilimia 84 katika mwaka 2007. Hata hivyo kwa upande
wa sekondari, uandikishaji umetajwa kuongezeka kutoka asilimia 15, mwaka
2007 mpaka 29, mwaka 2012
No comments:
Post a Comment