Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu wake Mahmoud
Mgimwa wakimsikiliza kwa makini Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa
wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa alipokuwa akitoa CD bungeni aliyodai
inaonyesha moja ya kampuni inayofanya uwindaji haramu kwenye baadhi ya
mbuga za wanyama nchini. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni imesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaongozwa kwa
ubabaishaji na ‘mvutano wa kimasilahi’ baina ya waziri na katibu mkuu,
hivyo kukwamisha shughuli za kuendeleza utalii.
Msemaji wa kambi hiyo (Maliasili na Utalii), Mchungaji Peter Msigwa
alitoa kauli hiyo juzi wakati akisoma maoni kuhusu hotuba ya Makadirio
ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.
Alisema kambi ya upinzani inasikitishwa na mvutano baina ya Waziri
Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarishi ambao unaonyesha
udhaifu wa Serikali.
“Hii inathibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, waziri na katibu
mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja
anaonekana kumvizia mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja
kutekeleza maazimio ya Bunge,” alisema Msigwa.
Alisema kitendo cha Waziri Nyalandu kuwasimamisha kazi wakurugenzi
wawili, lakini wakarudishwa na katibu mkuu huku akisema taratibu za
kuwafukuza hazikufuatwa na hii ni dalili kuwa hata yeye (Nyalandu) siyo
msafi kwa kuwa anashindwa hata kujua mipaka yake ya kazi.
Mbali na mvutano huo, Msigwa alisema maazimio ya Bunge kuhusu matokeo ya
Operesheni Tokomeza Ujangili yanaendelea kupuuzwa na watumishi wenye
tuhuma wakihamishwa vitengo.
“Ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki na
debe tupu haliachi kutika (siyo maneno yangu, bali ya wahenga). Siyo
mara ya kwanza kambi ya upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro
Nyalandu,” alisema.
Alisema Waziri Nyalandu alipozungumza katika kikao cha wadau wa ulinzi
wa maliasili Juni mwaka jana mkoani Iringa, aliahidi kuwa majina ya
majangili yakiwamo ya vigogo yangetangazwa hadharani, lakini hadi sasa
hakuna majina yoyote yaliyotangazwa hadharani.
Uteuzi wa Sarakikya
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) alizungumzia
kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi ya
Mkurugenzi wa Wanyamapori, jambo alilosema ni kinyume na haki za
binadamu.
Msemaji huyo alibainisha kuwa, wakati wote Watanzania wanajiuliza
maswali ambayo hayajapata majibu kuhusu vigezo vilivyotumika kumteua
Sarakikya.
“Katika Operesheni Tokomeza, mtu huyu alikuwa kiongozi wa utekelezaji wa
moja kwa moja na kinachodaiwa ni uvunjifu wa haki za binadamu,
inashangaza kuona mtu huyu tena ndiye ana nafasi ya kukaimu ukurugenzi,
lini kawa msafi?” alihoji Msigwa.
Msigwa pia alizungumzia shehena ya meno ya tembo ambayo alisema Serikali
inatafuta soko lake badala ya kuyateketeza kwa kuwa kuuza ni kuchochea
ujangili nchini.
Kudharau Mahakama
Msigwa alisema Mkurugenzi wa Wanyamapori alipuuza uamuzi wa Mahakama
ulioizuia Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris Limited kuwinda
baada ya kubainika inavunja sheria.
Msigwa alisema kuna taarifa kuwa kampuni hiyo ilishapewa zuio na
mahakama la kufanya uwindaji kutokana na kutozingatia sheria, lakini
ilipitia mlango wa nyuma na kuomba kibali cha uwindaji na kupewa.
Ajibu hoja
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge jana jioni, Nyalandu alisema Serikali
itachukua vielelezo vyote vya Msigwa kuhusu Kampuni ya Green Miles
Safaris Limited kufanya shughuli zake kinyume cha sheria na kuvifanyia
kazi.
Kwa upande wa wakurugenzi wizarani, alisema kuna upotoshaji wa baadhi ya
vyombo vya habari kwa kuwa hakuna mfanyakazi aliyefukuzwa kazi. ..
“Siyo Mkurugenzi Bwana Songorwa (Alexander) wala mtumishi mwingine.”
Alisema hatua aliyochukua ni kuwahamisha vituo vya kazi, Profesa
Songorwa alipelekwa Chuo cha Mwika kuwa mwalimu wakati Profesa Jaffar
Kidegesho alihamishiwa Hifadhi ya Selous.
“Sheria ya utumishi wa umma haikuvunjwa wala kanuni zake, naomba
nilithibitishie Bunge lako kuwa habari hizi nyingi za kwenye magazeti
hazikuwa na usahihi wowote,” alisema.
Akizungumzia shutuma za Kambi Rasmi ya Upinzani juu ya kuteuliwa kwa
Sarakikya kuwa Kaimu Mkurugenzi Wanyamapori, Nyalandu alisema hakuna
anayeweza kuyaelewa yote yaliyotokea katika Operesheni Tokomeza ila hadi
hapo Tume ya Kimahakama itakapokamilisha kazi yake.
“Ndugu Sarakikya ni mmoja watumishi waandamizi na waliobobea katika kazi
walizofanya… Kwa hali yoyote ile Serikali haitamwonea mtu haya endapo
atabainika na tume hii kwamba alivunja maadili yake,” alisema.
Ingawa Nyalandu hakujibu kuhusu uhusiano wake kikazi na Katibu Mkuu
Tarishi, baada ya bajeti yake kupitishwa Spika wa Bunge, Anne Makinda
alisema yamezungumzwa mambo mengi kuhusu suala hilo, hivyo inaonyesha
kuna tatizo.
Makinda alishauri waziri kuyo na katibu mkuu wake washirikiane ili kutimiza malengo ya Serikali
No comments:
Post a Comment