Mwananchi lilizungumza na baadhi ya wafanyabiashara ya ngono jijini
katika maeneo ya Mwananyamala Hospitali, Komakoma na Vingunguti ambao
walisema kuwa wanatumia dawa hizo kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya VVU
ili kuwaridhisha wateja wasiopendelea mipira hiyo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walidai kuwa wanatumia Truvada kuzuia
maambukizi pindi wanapokutana na wanaume wakware ambao huwabaka au
kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga.
“Hizi dawa tunazipata katika hospitali na wakati mwingine katika maduka
makubwa ya dawa. Kwa sababu zinazuia maambukizi ya Ukimwi na sisi ni
watu ambao tunafanya kazi katika mazingira hatarishi,” anasema Leyla
Musa, mmoja wa wanawake hao.
Si hivyo tu, kwa kuwa hii ni biashara baadhi yao hukubali kufanya
mapenzi bila mipira ili kupata fedha nyingi kutoka kwa wanaume.
Wengine hukimbilia huduma ya PEP
Baadhi ya wanawake hao wanasema kuwa baada ya kufanya mapenzi na wanaume
kadhaa asubuhi huenda katika kliniki zinazotoa huduma za ARV na
kudanganya kuwa wamebakwa na kisha hupewa huduma za dharura za ARV
zinazoitwa kwa kitaalamu Post-exposure prophylaxis.
Kwa kawaida mtu aliyebakwa au kujikata hupewa dawa aina ya Lamivudine, Zerophidine au Truvada kulingana na uzito wa tatizo.
“Tunatumia hizi dawa mara kwa mara lakini tunafanya hivyo katika kliniki
tofauti ili tusigundulike,” alisema mmoja wao, mkazi wa Mwananyamala,
Mariam Leshaniki.
Kwa maelezo ya Dk Rachel Baggaley, mtaalamu wa masuala ya Ukimwi wa
Shirika la Afya Duniani anasema dawa za PEP zipo maeneo mengi duniani
kwa sasa na zinafanya kazi kwa ufanisi pia hazina madhara kwa mwanamke.
“Dawa hizi siyo sumu mwilini, zinaingia kwenye mfumo wako wa damu kabla
virusi havijajizatiti na inavizuia ili mradi uzitumie ndani ya saa 72,”
anasema Dk Baggaley.
Dawa ya Truvada, ambayo ina mchanganyiko wa dawa aina ya Tenovofir na
Emtricitabine, imethibitishwa kuwa salama kwa kupunguza makali ya VVU
pia kuzuia maambukizi mapya. Dawa hizi zinazotengenezwa nchini India,
zimekuwa msaada mkubwa wa tiba kwenye nchi zinazoendelea.
Mkurugenzi wa Sera, Mpango na Utafiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk Raphael Kalinga alisema Tume hiyo inakemea
kwa nguvu zote tabia inayofanywa na watu hao, kwani hakuna tofauti na
kuvaa chuma kisha kujitumbukiza kwenye moto uwakao.
“Wanachofanya siyo sahihi. Ina maana kama una kinga ya malaria basi
unatakiwa ukae karibu na mbu wakuume. Si unawakimbia… huo siyo uamuzi
sahihi kabisa na ninawataka waondokane na tabia hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Dk Kalinga alikiri kuwa ni kweli dawa hizo zinazuia
maambukizi, lakini bado inategemea wingi wa virusi alivyonavyo mgonjwa
pia mtu anaweza kuambukizwa magonjwa mengine ya zinaa kama kisonono,
kaswende na pangusa.
“Kwa kweli tunakemea kwa nguvu zote na tunawashauri kwa usalama wao
waondokane na mawazo hayo na wala wasijaribu hata mara moja kuacha
kutumia kondom kuzuia maambukizi,” alisema.
Kama njia hii ya kuzuia maambukizi ya VVU itaendelea kufuatwa basi
itabadilisha mfumo mzima wa kupambana na virusi hivyo ambao unahimiza
matumizi ya kondomu kama kinga. Tangu mwaka 2010, tafiti tatu tofauti
kuhusu dawa ya Truvada zimefanyika na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzuia
maambukizi ya VVU iwapo zitanywewa kila siku. Wanaume wanaofanya mapenzi
ya jinsi moja waliotumia dawa hizo kila siku, walipopimwa damu
walionekana kuwa salama kwa asilimia 99.
Wakati Dk Kalinga akipinga matumizi ya Truvada kama kinga ya VVU,
Daktari wa magonjwa ya kuambukiza wa New York, Anthony Fauci, alisema ni
vyema dunia nzima ikakubaliana na mpango wa kuanza kutumia dawa hizo
ili kuokoa mamia ya watu walio katika hatari ya maambukizi.
“Kaswende, kisonono kinaweza kutibiwa na dawa za viua sumu
(antibiotics), lakini Ukimwi ukiupata ni wa maisha yote hauwezi
kutibiwa,” alisema Dk Fauci.
Kituo cha Kuzuia Magonjwa cha Marekani, kinaeleza kuwa hata kama
itakubaliwa Truvada zitumike kama kinga, basi zitatolewa kwa wale ambao
bado hawajaambukizwa. Pia, watatakiwa kupimwa kila baada ya miezi mitatu
kuhakikisha kuwa hawajapata maambukizo na kupimwa ili kujua kama
hawapati madhara yoyote yanayosababishwa na dawa hizo pia kama hawana
magonjwa ya zinaa.
Watafiti waliogundua Truvada wanaeleza kuwa dawa hiyo kwa sehemu kubwa
inakinga VVU na upande mwingine inasaidia kuua virusi vya Ukimwi kwa mtu
ambaye tayari ameshaathirika. Hata hivyo, FDA na watafiti hao
hawajaeleza kama Truvada inatibu moja kwa moja, isipokuwa wanasisitiza:
“Inamkinga mtu kupata maambukizi mapya, inamsaidia mwathirika kwa kuua
VVU pamoja na kumkinga dhidi ya magonjwa nyemelezi.”
Mtafiti wa Masuala ya Ukimwi, Dk Edward Maswanya anakana kuwa Truvada
inazuia maambukizi na kusema siyo sahihi kutumia dawa hizo kama kinga.
“Kinga inayoaminika na kukubalika kuzuia maambukizi ni kondomu pekee hiyo Truvada haizuii kabisa,” alisema.
Alisema wanaofanya biashara ya ukahaba wanajiweka hatarini kupata maambukizi ya VVU pia wapo hatarini kuambukiza wengine.
Baadhi ya wanawake wanaofanya biashara ya ngono wa eneo la Temeke,
Tandika na Mbagala Zakhem walipohojiwa walidai kuwa mipira ya kiume
imekuwa siyo salama kwao tena, kwani kuna wakati wanaume huitoboa kwenye
chuchu na mara nyingine huzama ukeni kiasi cha kusababisha wafanyiwe
upasuaji.
“Kondomu zinasaidia, lakini kwa wanaume wastaarabu, lakini ninapomeza
hizi dawa hata nikibakwa zinazuia maambukizi na zinasaidia kama ninao
nisiwaambukize,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Mashoga nao
Mwanamume anayeshiriki mapenzi ya jinsi moja, Aly maarufu kama Aunt Aly,
mkazi wa Kinondoni anasema ingawa anaishi na VVU, lakini yeye huzitumia
dawa hizo kuepuka kupata maambukizi mapya na kuzuia asiwaambukize
wengine, kwani hubakwa mara kwa mara na vibaka.
No comments:
Post a Comment