WABUNGE wa Kambi Rasmi ya Upinzani, jana walitoka nje ya ukumbi wa
Bunge, kususia uhitimishaji wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini.
Wabunge hao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), waliamua
kususia mjadala huo kwa madai ya kutoridhishwa na ulivyokuwa ukiendeshwa
kwa mikakati waliyowekeana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya
kufukia kashfa nzito ya IPTL inayoikabili wizara hiyo.
Kabla ya kutoka nje ya Bunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani,
Freeman Mbowe (CHADEMA), alisema hawako tayari kuendelea kushirikiana
mjadala huo wakati tayari CCM na serikali yake wameshaweka msimamo wa
kuwazomea na kupinga kila hoja ya wabunge wa upinzani.
Mbowe, alisema amefuatilia mjadala huo, lakini kwa bahati mbaya umegubikwa na minyukano ya kiitikadi na makundi.
Alisema wabunge wanajadili kwa kujaribu kufukia mambo mazito kwa sababu
ya mitazamo ya makundi na kiitikadi, hivyo sio busara kuendelea
kushiriki.
“Mheshimiwa Spika, nashawishika kabisa kusema kuendelea kushiriki
mjadala huu ni sawa na kutowatendea haki wananchi wetu, sina matatizo na
Waziri Muhongo, wala katibu wake, tatizo langu ni mfumo. Waheshimiwa
wabunge, hebu someni hotuba yetu mjue tunasema nini.
“Watu hamsomi, hamfanyi utafiti, lakini mmeshaweka misimamo kwa kutumia
uwingi wenu, hatuwezi kushiriki mjadala kama huu tunapoona mambo
yanachakachuliwa waziwazi, kuendelea kushiriki mjadala huu ni kulinajisi
taifa, ni bora tuwaachie mjadala huu muhitimishe nia yenu kwa raha,”
alisema Mbowe.
Huku akizomewa na wabunge wa CCM, Mbowe alisema wizara hii ina kashfa
kubwa ya IPTL, na kuna ripoti nyingi ya tume zilizoundwa na maazimio ya
Bunge, lakini yameendelea kukaliwa bila sababu.
Baada ya kauli hiyo, Mbowe, alianza kutoka nje na kufuatiwa na wabunge wote wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Wakati wanatoka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, alisema wabunge hao wametoka kuhofia majibu ya Waziri
Muhongo.
“Wao wanasema sisi tumepanga mikakati, sio kweli, wao ndio waliopanga
mchana huu kwamba watoke kumhofia Muhongo,” alisema Lukuvi.
Nje ya Bunge
Akizungumza na waandishi katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Mbowe alisema
wametoka kwa sababu tatu ambazo ni pamoja na CCM kupanga mkakati wa
kuwazomea wakati Waziri Muhongo atakapokuwa anahitimisha hoja yake.
Pili alisema wabunge wa upinzani John Mnyika na David Kafulila,
walipojaribu kuibua hoja ya kashfa ya ITPL, walilazimishwa kutoa
ushahidi hapo hapo kwa lengo la kuwatisha, na wamepanga kukataa hoja ya
kutaka iundwe Kamati Teule kuchunguza kashfa hiyo.
Kwa mujibu wa Mbowe, sababu ya tatu ni wizara hiyo kukalia ripoti za tume na maazimio mbalimbali ya Bunge.
Alisema Bunge limekalia ripoti ya Jairo, ripoti ya tume iliyoenda
kuchunguza vurugu Mtwara, imezima utekelezaji wa maazimio ya kashfa ya
Richmond.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe, alisema hawako tayari kuendelea kushiriki
kwenye mjadala huo na wametoka ili kuionyesha dunia kwamba kuna tatizo
ndani ya Bunge.
Hata hivyo, alisema leo wataendelea na mjadala wa Bunge la Bajeti kwani
walitaka kupitisha ujumbe wao kupitia wizara hiyo ya Nishati na Madini.
Juzi usiku, CCM walikuwa na kikao na kukubaliana kuilinda wizara hiyo kwa gharama zozote.
Hata hivyo, wakati wa majumuisho ya hoja za bajeti hiyo, Naibu Waziri wa
Nishati na Madini Stephen Masele, alimlaumu balozi wa Uingereza hapa
nchini kuendesha vitendo vya kuihujumu, ikiwemo kuzungumza na wadau
mbalimbali ili wazuie Tanzania isipate misaada.
Alisema kuwa wana ushahidi mzito kuwa balozi huyo amekuwa akiitaka
serikali ilipe deni la benki ya Standard Charter inayoidai kampuni ya
kufua umeme wa dharura ya IPTL, lakini Tanzania imepinga malipo hayo.
Alibainisha kuwa serikali inamtaka balozi huyo afike Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kujibu tuhuma hizo na ajipime kama
anafaa kuendelea kutumikia nafasi hiyo hapa nchini.
CREDIT:MTANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment